Wakulima wa Matunda Njombe Kujengewa Uwezo



Mkulima wa kupigiwa mfano wa kilimo cha Maparachichi Mkoani Njombe, Bw. Reuben Mtitu (kulia) akizungumza na Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) walipomtembelea shamba lake mkoani Njombe kujionea maendeleo ya miradi iliyokopeshwa na Benki hiyo. Pichani ni Kiongozi wa Msafara huo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib (mwenye miwani) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo (watatu kulia). Wengine ni Mrajis Msaidizi wa Ushirika wa Mkoa wa Njombe, Bw. Exaud Sepali (kushoto) na Meneja Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe (mwenye kofia).


Kiongozi wa Msafara wa Ukaguzi wa Miradi ya Kilimo Mkoani Njombe ambaye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib (Kushoto) akiwa na msafara wa ukaguzi wa miradi inayokopeshwa na Benki ya Kilimo wakishuhudia chanzo cha maji kinachotumika kumwagilia zao la maparachichi mkoani Njombe. Wengine pichani ni Mrajis Msaidizi wa Ushirika wa Mkoa wa Njombe, Bw. Exaud Sepali (wapili kulia), Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo (wapili kushoto) na Meneja Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe (kushoto).




Na mwandishi wetu, Njombe

Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imesema ipo tayari kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya usindikaji wa Matunda kwa ajili ya kuongeza thamani kwa wakulima wa matunda wa Mkoa wa Njombe ili kukidhi masoko.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib wakati akizungumza na Umoja wa Wakulima wa Wanajombe AMCOS wakati wa Ziara ya kutembelea miradi ya kilimo inayowezeshwa na Benki ya Kilimo Mkoani Njombe.

Bibi Twalib alisema kuwa TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini hasa kwa wakulima wadogo kwa lengo la kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

“Benki imejipanga katika kusaidia kuchagiza kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima mkoani Njombe na Tanzania kwa ujumla,” alisema.

Aliongeza kuwa Benki ya Kilimo ipo tayari kusaidia kukabiliana na mapungufu katika uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya usindikaji wa Matunda kwa ajili ya kuongeza thamani.

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Ushirika wa Mkoa wa Njombe, Bw. Exaud Sepali alisema kuwa Wananjombe wanataka kutumia fursa za mikopo nafuu kutoka Benki ya Kilimo ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa uendelezaji wa viwanda vya kusindika mazao unafanyika kwa uhakika.

“Fursa za mikopo ya TADB inatupa nafasi ya kupewa mkopo kwa ajili ya kupata mtaji kwa ajili ya uendeshaji, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi na masoko zitakazotuwezesha kujenga viwanda vya kusindika matunda ambayo yanalimwa kwa wingi mkoani Njombe hali itakayotuhakikishia uendelezaji wa wakulima wetu,” alisema.

Naye, Meneja Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe alisema kuwa kwa upande wa miundombinu ya masoko, Benki ya Kilimo inatoa mikopo kwa minyororo ya thamani kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya masoko kama vile ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mahindi na miundombinu ya masoko na kugharamia usafirishaji wa malighafi na nmatunda yaliyoo tayari kwenda sokoni.

Aliongeza kuwa Mnyororo wa thamani wa Kilimo cha Matunda ni miongoni mwa minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao mbalimbali. Maeneo yanayowekewa mkazo kwenye Mnyororo wa thamani wa Kilimo cha Matunda ni pamoja na Uongezaji Tija wa Kilimo cha Matunda na Miundombinu ya masoko.

“Pia Benki inagharamia uanzishaji wa mifumo ya upatikanaji wa taarifa za masoko pamoja na kuwezesha uhusiano wa masoko ya ndani na masoko ya kikanda na kugharamia mahitaji mengineyo ya kuwezesha miundombinu ya masoko,” aliongeza Bw. Pangamawe.

Aliongeza kuwa Dira ya Benki ya kilimo ni kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

No comments:

Post a Comment

Pages