Tanzania Yashinda Tuzo Ya Umoja Wa Mataifa Ya Ubunifu Bora Katika Huduma Za Umma Kupitia Mfumo Wa E-Mrejesho.

 Tuzo za Umoja wa Mataifa za Ubunifu katika Huduma za Umma 'UN Public Service Innovation Awards' zimetolewa leo Juni 26 mwaka huu, nchini Korea Kusini kwenye Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma ya Umoja wa Mataifa 'UN Public Service Week 2024'.


Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 72 zimeshiriki ambapo mifumo 400 iliwasilishwa na mifumo 15 ukiwemo wa e-Mrejesho ilishinda tuzo mbalimbali ambapo, kutoka Afrika nchi zilizoshiriki na kushinda tuzo hizo ni Tanzania na Afrika Kusini pekee.

Mfumo wa e-Mrejesho unawawezesha wananchi kutuma kero au malalamiko, maoni, maswali, na pongezi kidijiti kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kupata mrejesho wa utekelezaji wake kidijiti mahali walipo.

Mfumo huu umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni tumizi (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya e-mrejesho.gov.go.tz.

Wiki ya Utumishi wa Umma ya Umoja wa Mataifa ni tukio la kila mwaka linaloadhimishwa kimataifa, kwa lengo la kusherehekea thamani na umuhimu wa huduma ya umma kwa jamii.

Tukio hili linasisitiza kutambua mchango wa watumishi wa umma na kuhamasisha vijana kuchagua kazi katika sekta ya umma.

Wiki hii kwa kawaida hujumuisha matukio, sherehe za tuzo, na majadiliano kuhusu jinsi ya kuboresha ufanisi wa utoaji huduma kwa umma duniani kote.





Comments

Popular posts from this blog

ANGALIA HAPA, FAIDA ZA MBEGU ZA MABOGA

SERIKALI YAFUNGA KIWANDA KWA SIKU 14 NA KUVITOZA FAINI YA JUMLA YA SH. MILIONI 40.8 VINGINE VITATU JIJINI DAR ES SALAAM

UZINDUZI WA KIWANDA CHA AZAM DAIRY PRODUCTS LIMITED FUMBA