Umeisikia kampeni ya EATV, East Africa Radio iitwayo “Zamu Yako 2015″?

KITUO cha Televisheni chenye ushawishi mkubwa kwa vijana  nchini Tanzania, EATV, sambamba na kituo chake cha East Africa Radio,  mapema leo wamezindua rasmi kampeni kubwa na ya aina yake ijulikanayo kwa jina la ZAMU YAKO 2015.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa vipindi East Africa Radio, Nasser Kingu alibainisha kampeni hiyo inamalengo mahususi kwa Taifa ikiwemo vijana kwa ujumla juu ya kuwakumbusha na kuwaelimisha vijana kuhusiana na umuhimu pamoja na uwezo walionao katika kufanya maamuzi sahihi kwenye masuala makubwa ya kitaifa hususani yanayohusu siasa za Tanzania.
“Kampeni hii ina dhamira ya kuhimiza vijana kutumia fursa waliyonayo katika kufanya maamuzi na mambo mbalimbali.
Kwanza kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ya maoni katika  mchakato wa kutafuta katiba mpya, na mwisho kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura ili kuchagua viongozi wao ambao ni madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alibainisha Kingu.
Aidha Kingu alisema EATV na East Africa Radio, imekuwa na mvuto mkubwa sana kwa vijana hivyo lengo la kampeni hiyo itafanikiwa kwani inawalenga na kuwagusa moja kwa moja vijana.
Kingu pia aliweza kutoa takwimu kadhaa, ambapo alisema kwa Tanzania, umri rasmi wa kupiga kura ni kuanzia miaka 18 na kuendelea, kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012, Jumla ya watu Milioni 22, (22,424,136) wanatazamiwa  kushiriki zoezi hilo kwa mwaka huu.
“Katika idadi hiyo ya wapiga kura, vijana wenye umri wa miaka 18 mpaka 40 peke yao  ni 15,293,681. Idadi ambayo ni sawa na asilimia 68.20 ya wapiga kura wote.
Hii ina maanisha kwamba hatma ama mustakabali wa Taifa hili uko mikononi mwa vijana. Na ndio maana vituo vyetu Tv na Radio vinaaminika zaidi na vijana,  hivyo tunaendesha kampeni hii kwa kutambua umuhimu na nguvu ya vijana katika taifa letu.
Ikumbukwe pia hii si mara ya kwanza kwa vituo vyetu kuwa na kampeni kama hii, mwaka 2010, tulikuwa na kampeni ya kuwataka vijana kuacha kulalamika  na kutumia kura yao” alifafanua Kingu.
Kampeni hiyo inatarajiwa kufanywa na vituo hivyo kupitia vipindi vyao mbalimbali kila siku, ikiwemo kufanya mahojiano na wananchi, vijana, vingozi wanasiasa, watu maalufu na wengineo wengi ambao pia watakuwa wakialikwa kwenye studio za vipindi vya vituo hivyo, kwa zaidi ya mwaka mzima.
DSCN9941
Mkuu wa vipindi wa East Africa Radio, Nasser Kingu (kushoto) akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kuzindua kampeni ya Zamu yako 2015, Kulia kwake ni Mkuu wa Masoko Eatv & East Africa Radio, Alex Galinoma

Post a Comment

0 Comments