Mkuu
wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Rosalynn
Mworia (katikati),akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawamo
pichani) wakati wa kutangaza ushirikiano wa kimkakati na Benki Tarajiwa
ya Walimu (Mwalimu Commercial Bank in-formation) kurahisisha ununuaji
hisa kupitia huduma ya M-Pesa pamoja na kampuni ya Maxcom Africa kupitia
huduma yake ya Maxmalipo, Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo
Ronald Manongi na kulia ni Ofisa Mkuu wa Maswala ya Biashara wa Max
Malipo Ahmed Lussasi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mwalimu Commercial Bank (in-formation), Ronald Manongi na
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Rosalynn
Mworia (kushoto) wakipeana mikono ikiwa ishara ya uzinduzi wa
ushirikiano wa kimkakati na Benki hiyo kurahisisha ununuaji hisa kupitia
huduma ya M-Pesa pamoja na kampuni ya Maxcom Africa kupitia huduma yake
ya Max Malipo. Wengine katika picha wapili kushoto ni Ofisa Mkuu wa
Maswala ya Biashara wa Max Malipo Ahmed Lussasi na Mwekahazina Mkuu wa
Benki hiyo Nunu Saghaf.
Dar es
Salaam, 22 Aprili, 2015 – Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambao ni
waanzilishi wa Benki Tarajiwa ya Walimu (Mwalimu Commercial Bank
in-formation), kinawatangazia Walimu na Watanzania wote kwa ujumla juu
ya uuzwaji wa Hisa za Benki tarajiwa ya Walimu, kwa lengo la kupanua
wigo wa wanahisa na kuongeza mtaji ulianza tarehe 23 Machi 2015 na
unategemea kumalizika tarehe 4 Mei 2015.
Ili
kufikia azma hii, pamoja na njia nyingine za uuzaji wa Hisa zake, Benki
Tarajiwa ya Walimu inatangaza ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya
mawasiliano ya Vodacom kupitia huduma yake ya M-Pesa pamoja na kampuni
ya Maxcom Africa kupitia huduma yake ya Maxmalipo.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
na Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia alisema,
“Tunafahamu umuhimu wa kuwezesha Walimu na Watanzania wote kununua hisa
kwa urahisi kabisa bila kutoa mguu majumbani kwao na hivyo tumeamua
kushirikiana na Benki Tarajiwa ya Walimu kurahisisha zoezi hili la
ununuaji hisa kupitia huduma yetu ya M-Pesa inayopatikana nchini kote
kupitia mtandao wa mawakala zaidi ya 85,000.”
Vodacom
kupitia huduma yake ya M-Pesa imerahisisha ununuzi wa hisa kupitia simu
za mkononi kwa kuondoa adha ya usajili. Mteja anapoingiza namba yake ya
simu kama namba ya kumbukumbu moja kwa moja taarifa zake zinaingizwa
kwenye rekodi kupitia mifumo ya Maxcom Africa.
Sasa
hatua za usajili na manunuzi zimeunganishwa katika mchakato mmoja
kupitia huduma hii ya M-Pesa. Ili kufanya manunuzi ya hisa mteja
anatakiwa kupiga *150*00# kupata menu ya M-Pesa na kisha kuchagua “Lipa
Kwa M-Pesa” halafu achague Namba ya Kampuni na kisha ingiza 236622 kama
Namba ya Kampuni. Hatua inyofuata ni kuingiza namba ya simu kama
kumbukumbu ya malipo na kisha kiasi anacholipia kulingana na idadi ya
hisa alizonunua. Hatua ya mwisho ni kuweka PIN ya M-Pesa na kisha
Kamilisha Muamala.
Hisa
moja itauzwa kwa shilingi mia tano tu (Tsh. 500/-) na kiwango cha chini
cha manunuzi ya Hisa ni Hisa mia moja (100) sawa na shilingi elfu
hamsini (Tsh. 50,000/-) na baada ya hapo unaweza kununua Hisa hizi kadri
ya uwezo wako.
“Tulipozindua
ununuzi wa hisa za Benki Tarajiwa ya Walimu mnamo Machi 23, 2015
tulitumia mfumo ambao ulihitaji mteja kujisajili kwanza kabla ya kununua
hisa lakini sasa M-Pesa imerahisisha zoezi hili kwa kuondoa hatua ya
usajili. Tunatumaini kuwa sasa tutaweza kupata idadi ya wanahisa
wasiopungua laki tatu kama tulivyopanga hapo awali,” alisema Rais wa
Chama cha Walimu Tanzania, Mwalimu Gratian Mukoba
“Tunawahakikishia
Walimu na Watanzania wote kuwa huduma hii ni rahisi sana, ya uhakika na
salama kabisa kama ambavyo miamala mingine inayopitia huduma ya M-Pesa
ilivyo salama,” aliongeza.
Nia na
madhumuni ya ushirikiano huu wa kihistoria ni kurahisisha uuzwaji wa
Hisa za Benki Tarajiwa ya Walimu na kutoa fursa hii adimu kwa Walimu
zaidi ya laki mbili na mamilioni ya Watanzania kumiliki Benki na hivyo
kujumuishwa katika uchumi wa kisasa kwa nia ya kuboresha maisha yao.
Naye
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)
Bibi Nasama Massinda alisema kuwa juhudi za Mamlaka hiyo za kuwezesha
wananchi wengi kushiriki katika masoko ya mitaji kwa kununua hisa
zilikwama kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali.
Ushirikiano
huu wa leo kati ya mwekezaji yaani Benki Tarajiwa ya Walimu na kampuni
za Vodacom Tanzania na Maxcom Africa ni mafanikio makubwa yaliyotokana
na ya utekelezaji wa utaratibu wa kuwezesha wawekezaji kushiriki katika
masoko ya mitaji kwa kutumia teknolojia kupitia Miongozo ya Uuzaji na
Ununuzi wa Hisa kwa Njia ya Teknolojia ya Mawasiliano (Capital Markets
and Securities Electronic Trading Guidelines, 2015).
“Sasa
mwalimu anaweza kununua hisa huku akiendelea kusahihisha madaftari ya
wanafunzi katika kituo chake cha kazi popote alipo iwe mjini au
kijijini. Kwa kuwa uuzaji wa hisa za benki tarajiwa ya Mwalimu uko wazi
kwa watu wote, hivyo basi kwa mara ya kwanza katika nchi yetu wananchi
wanaweza kununua hisa katika soko la awali kupitia teknolojia ya simu za
mikononi.
“Haya
ni mageuzi makubwa katika maendeleo ya masoko ya mitaji kwani, Mamlaka
ya Masoko ya Mitaji ya Tanzania inaweka historia kwa kuwa Mamlaka ya
kwanza katika nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki (EAC) kwa kuwezesha
ununuzi wa hisa katika soko la awali (IPO) kwa kupitia simu za
mkononi,’’ aliongeza.
Katika
kuweka kwa vitendo yaliyozungumzwa hapo juu na viongozi hao, Benki
Tarajiwa ya Walimu na Vodacom kwa kushirikiana na MaxMalipo kwa pamoja
watafanya kampeni ya uhamasishaji wa uuzwaji wa Hisa za Benki Tarajiwa
ya Walimu kupitia huduma ya M-Pesa ambayo imewezesha kuboreshwa zaidi
kwa mchakato wa ununuzi wa Hisa ili kukidhi mahitaji ya wanunuzi.
MaxMalipo watatoa msaada na huduma kwa wateja kwa saa 24 kupitia namba 0764 700 200.
Mbali
na M-Pesa unaweza kununua Hisa za Benki Tarajiwa ya Walimu kupitia
mawakala wa Maxmalipo wanaopatikana kote nchini na katika ofisi zote za
posta, matawi yote ya Benki ya CRDB nchini na mawakala wote wa Soko la
Hisa la Dar es Salaam.
0 Comments