Vodacom Foundation yakabidhi msaada wa Umeme Jua kwa wahanga wa mvua Kahama


Mkuu wa Vodacom Tanzania,Kanda ya Tanganyika George Venanty(kushoto) na Meneja Masoko wa Kampuni ya Associate AEG Winnie Nyamubi(kulia) wakielezea matumizi ya Umeme Jua”Solar Power” wakati wakukabidhi msaada huo uliotolewa na Vodacom Foundation kwa wahanga wa maafa ya mvua kwenye kijiji cha mwakata wilayani Kahama Mkoani Shinyanga mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga(kulia) akipokea msaada wa Umeme Jua ”Solar Power”kwa niaba ya wahanga wa maafa ya mvua uliotolewa na Vodacom Foundation kutoka kwa Mkuu wa Vodacom kanda ya Tanganyika,George Venanty.

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii “Vodacom Foundation” leo imekabidhi msaada kwa wahanga wa mvua wa Kahama mkoani Shinyanga. Msaada huo unatokana na mchango wa kampuni na michango ya wateja wake walioguswa na tukio hilo kupitia  namba  maalumu ya kupokea msaada ya kusaidia majanga mbalimbali ya 155990.

Mvua kubwa iliyonyesha wilayani Kahama mkoani Shinyanga mapema mwezi uliopita ilisababisha vifo vya watu 42 na wengine mamia kujeruhiwa na kuacha familia nyingi zikiwa hazina makazi.

Baada ya tukio hilo Vodacom ilitangaza kutoa mchango wa kuwasaidia wahanga hao na iliwaomba wateja wasaidie kuchangia  kupitia namba maalumu ya kupokea misaada ambapo  wateja walichangia na kuweza kupatikana kwa ajili ya kuwapatia msaada wahanga hao.

“Tunawashukuru wateja wetu wote walioguswa na tukio hili la kusikitisha kusaidia watanzania wenzetu wa  Kahama mkoani Shinyanga ambao ni wahanga wa mvua kubwa iliyonyesha kwenye eneo hilo na kusababisha maafa. Tunawaomba waendelee kuwa na moyo huu wa kusaidia wenzao katika kipindi kigumu cha matatizo” Alisema George Venanty Mkuu wa kanda hiyo kwa niaba ya Vodacom Foundation wakati wa makabidhiano ya msaada huo wa Umeme Jua”Solar Powar” kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Ally Rufunga kwa niaba ya wakazi wa Kahama.

Akipokea msaada huo Mkuu wa mkoa huo Ally Rufunga aliishukuru kampuni hiyo kwa kuona umuhimu wa kusaidia katika janga hili na aliwaomba wadau wengine wajitokeza kuendelea kusaidia. “Kwa kuwa janga lilikuwa kubwa wananchi wengi walipata athari mbali na waliopoteza maisha na kujeruhiwa, wengi  nyumba zao zilianguka na wakapoteza mali zao hivyo bado mpaka sasa wanahitaji kupata misaada mbalimbali ili maisha yao yaweze kuendelea kama kawaida” Alisema.

Kupitia njia hii ya namba maalumu ya kuchangisha fedha, Vodacom imewahi kurahishisha uchangishaji wa fedha kwa waathirika wa matukio yaliyotokea siku za nyuma na kuathiri wananchi. Moja ya matukio hayo ni milipuko ya mabomu ya Mbagala na Gongo la mboto jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages