KAMPUNI ya Simu za Mkononi Zantel imezindua Kampeni ya Jibwage na Mbuzi katika kusherehekea Sikukuu ya Idd el Adha, ikitambulika pia kama 'Sherehe ya Kuchinja' kwa kutoa mbuzi 500 kwa wateja wake wenye matumizi ya zaidi huku mbuzi 100 wakigawiwa katika vituo mbalimbali vya watoto yatima nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Benoit Janin amesema "Hii ni sehemu ya kuwashukuru wateja wetu na kusherehekea pamoja nao Sikukuu ya Idd. Imekuwa ni utamaduni wetu kurudisha katika jamii kupitia kampeni na miradi mbalimbali, hivyo kwa leo Zantel inatoa mbuzi 500 katika kusherehekea Sikukuu hii ya Kuchinja.”
Idd el –Adha ni moja ya sikukuu mbili muhimu za Kiislamu ambayo waumini wa dini ya kiislamu huiadhimisha kwa kuonyesha umuhimu wa kutoa sadaka kwa kuchinja na ibada.
Mbuzi 400 watatolewa kwa wateja wa Zantel wenye matumizi zaidi kuliko wengine na ambao watakuwa wamejisajili katika kampeni kwa kupitia *149*15# na kuchagua “Jibwage na Mbuzi”. Kujisajili katika promosheni hii ni bure kwa wateja wote wa Zantel. Kila siku wateja 40 watakaokuwa wametumia muda zaidi watajizawadia mbuzi.
“Hii si bahati nasibu, wale wateja wa juu watakaokuwa wametumia dakika nyingi bila kuchezeshwa mchezo wa bahati watakuwa wamejizawadia moja kwa moja hivyo natumia fursa hii kuwahamasisha wateja wetu kujisajili ili kupata mbuzi na kusambaza furaha ya Eid katika familia zao” alisema Benoit
Mbuzi 100 wanaobaki watatolewa msaada kwa vituo vya watoto yatima vilivyochaguliwa katika mikoa mbalimbali.
“ Pia tunatumia nafasi hiyo hiyo kusaidia watoto yatima na wale wasioweza kufanikisha sadaka hii ya kuchinja ili nao wafurahi pamoja na wengine na kushiriki upendo unaotokana na Idd”, ameongeza.
Miongoni mwa miradi ambayo Zantel imetoa misaada ni mradi wa kina mama wanaozalisha zao la mwani Unguja, huduma za maktaba Zanzibar –Zanzibar Library Services, vile vile kompyuta na internet ya bure kwa kikundi cha wasanii cha Mkubwa na Wanawe na vituo mbali mbali vya walimu Zanzibar.
0 Comments