TTCL YAZINDUA HUDUMA YA 4G ZANZIBAR



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti w Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu akiwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Waziri Waziri Kindamba wakinyanyua mabango ya matangazo kuashiria kuzinduliwa kwa huduma ya 4G ya Kmpuni hiyo Zanzibar (kushoto) Mkuu wa Kanda ya Zanzibar Franscis Mabula.


Na Khadija Khamis,
MAELEZO Zanzibar.





Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu amewataka wananchi kujiunga na huduma ya mawasiliano ya 4G LTE Zanzibar ambayo inauwezo mkubwa wa mawasiliano ya haraka .
Akizundua huduma za 4G LTE katika ofisi za Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) , Waziri Gavu alisema kwamba ukuaji wa teknolojia unawalazimu watumiaji wa simu za mkononi kuwa na mawasiliano ya uhakika.
Waziri Gavu alisema kwamba huduma hiyo itawarahisishia wananchi wa Zanzibar mawasiliano katika kazi zao za kilimo, biashara ufugaji pamoja na wafanyakazi wa serikalini na sekta binafsi.
“Teknolojia inaendelea kukua na kuja na ugunduzi mpya, nakuombeni wananchi wenzangu tutumie teknolojia hizi katika kuharakisha maendeleo yetu maana huduma za mawasiliano ni sehemu muhimu katika kuchapuza maendeleo” Alisema Waziri Gavu.
Alisema anaimani kuwa kuanza kutumia teknolojia hizo za 4G LTE kutawezesha sasa kuwaunganisha wananchi katika maeneo mbalimbali kimawasiliano ikiwa pamoja na kutumia huduma hizo katika kukuza biashara ya mtu mmoja mmoja au kikundi.
Waziri Gavu alisema kwamba Aidha sekta za serikali na binafsi zitaimarishwa kwa kupata huduma nzuri kutokana na mawasiliano ya 4G ambayo yamejipanga kwa mwaka mmoja tu kuenea kwa Tanzania nzima.
Nae Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema huduma ya mawasiliano ya 4G ina gharama nafuu kwa wateja wake,lakini pia mawasiliano yake ni ya uhakika zaidi.


“Mheshimiwa Waziri gharama za 4G ni shilingi moja kwa sekunde kwa mtumiaji, kiwango cha tozo hiki ni nafuu sana kulinganisha na kampuni nyengine hapa nchini.”Alieleza.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL alisema kwamba kuzinduliwa kwa huduma hizo wakati huu wa kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar ni kielelezo tosha cha namna TTCL inavyoenzi kwa vitendo Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo yaliwakomboa wananchi wa Visiwa hivi katika ukoloni mkongwe wa Kisultan.


“katika kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuweza kuungana na wenzetu kwa pamoja kitu kizuri cha kuwapa kama ni zawadi ni 4G ni mawasiliano yaliobora na ya kisasa “alisema Kindamba .
Aidha alisema huduma hizo ni kiungo muhimu katika kustawisha maendeleo ya jamii kupitia katika Nyanja zote ikiwemo kiuchumi kisiasa na kijamii.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, kauli mbiu yetu ya kutambulisha huduma za 4G LTE Zanzibar ni “Chei chei Zanzibar tumefanikisha” alisema Kindamba.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiunga na huduma za 4G LTE ikiwa ni kampuni ya kizalendo ya hapa Tanzania.
Alisema kuwa lengo kuu la kampuni hiyo ni kuifanya kampuni kuwa namba moja kwa Tanzania ambayo itatoa huduma ya simu ya mezani na mkononi na kurudi katika ubora wake wa awali na pia ni mdau wa TEHAMA.

No comments:

Post a Comment

Pages