Balozi wa Morocco atembelea TADB



Picha ya pamoja na Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na mara baada ya kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB.



Na mwandishi wetu,

Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane ametembelea Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano uliosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Morocco wakati wa Ziara ya Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI alipotembelea nchini Tanzania mwezi Oktaba mwaka jana.

Mheshimiwa Benryane ambaye alifuatana na uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM), ulioko nchini kwa ajili ya kikao cha pamoja cha ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kilimo inayotekelezwa kati ya Benki hiyo na TADB.

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB, Mheshimiwa Benryane alisema kuwa utekelezaji wa makubaliano kati ya Mfalme wa Morocco na Rais Dkt. John Pombe Magufuli yanaendelea vizuri na kutolea mfano mashirikiano kati ya benki hizo mbili kwa upande wa miradi ya kilimo.

“Ni chini ya mwaka mmoja tangu viongozi wetu wakubaliane utekelezaji wa mikataba 21 katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kilimo, gesi, madini na na usafiri wa anga,” amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga aliishukuru GCAM kuichagua TADB kusimamia miradi ya utekelezaji wa makubaliano hayo kwa upande wa kilimo.

Kwa mujibu wa Bw. Assenga, pamoja na kupanga mikakati hiyo, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua miradi kadhaa ya kilimo na ufugaji ambayo Tanzania inaweza kuianzisha kwa mafanikio.

TADB imeanzishwa kwa malengo makuu ya Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania; na Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

No comments:

Post a Comment

Pages